Header Ads

LEVANTE YAVUNJA MWIKO WA BACA,YAPIGWA 5-4,JE SIMBA SC NAYO ITAVUNJWA MWIKO WAKE?

Image result for BARCELONA

Hatimaye ilifika mwisho. Baada ya safari ndefu ya kucheza michezo 36 bila kufungwa kwenye La Liga, ilifika mwisho baada ya Barca kukubali kichapo cha mabao 5-4, mbele ya Levante. 

Ile ndoto ya kumaliza msimu bila kupoteza ikapotea kwenye mchezo wa 37. Mchezo mmoja kabla ya kumaliza msimu. Fedheha iliyoje hii. 

Ni straika Mghana, Emmanuel Boateng, ndiye aliyepeleka kilio kwa Barca baada ya kupachika mabao matatu katika mchezo huo na kufanya kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Phillipe Coutinho ionekane si lolote. 

Ni usiku huo Coutinho alifunga ‘hat trick’ yake ya kwanza akiwa Barca na ndiyo siku hiyo mashabiki wa Barca walipoteza rekodi yao. 



Ziko sababu tatu zilizopelekea kichapo hicho. 

01: Bila Messi, hakuna Barca 

Kosa kubwa la Ernesto Valverde ni kamari aliyoicheza kwa Lionel Messi. Si tu kwamba hakumpanga kwenye kikosi cha kwanza, bali hakumjumuisha kabisa Messi katika timu iliyosafiri kwenda kucheza na Levante. 

Hili liliwaumiza sana Barcelona na ndiyo sababu kubwa iliyowafanya washindwe kuifikia rekodi ya kumaliza msimu bila kufungwa. Tofauti ya Barcelona bora na mbovu ni Lionel Messi tu. 

Bila Messi, Barca ni timu tofauti kabisa na tuliyoizoea. Dhidi ya Levante ilionekana kabisa kuna kitu walikosa kila wanapovuka na mpira katika mstari wa katikati ya uwanja. 

Phillipe Coutinho na Luis Suarez walifanya kazi kubwa sana lakini haikusaidia kitu. Barca ilionyesha kumhitaji Messi ili kupata wanachokitaka. 

Unapokuwa na mchezaji aina ya Messi uwanjani unakuwa na uhakika wa kupata vitu viwili. Kama si pasi ya kutengeneza bao basi atafunga kwa juhudi zake mwenyewe. 

Kama kweli lengo la Valverde lilikuwa ni kumaliza msimu bila kufungwa, basi angemjumuisha Messi katika kikosi chake. 

Kama ni ngumu kumwanzisha basi angemweka hata benchi kwa ajili ya kuja kuokoa jahazi pindi linapozama. Alishawahi kufanya hivi kabla na alifanikiwa. Sijui kwanini ilishindikana dhidi ya Levante. Sijui kwa kweli. 

02: Yerry Mina bado sana 

Kamari ya pili aliyoicheza Ernesto Valverde ni kuwapanga Yerry Mina na Thomas Vermaelen kama mabeki wawili wa kati. Kamari ya kipuuzi kabisa. 

Mpaka dakika 20 za kipindi cha kwanza tayari Barcelona walikuwa wamesharuhusu mabao 2-0. Baada ya Vermaelen kupata majeraha na kutolewa, nafasi yake ilichukuliwa na Gerard Pique. 

Bado hakukuwa na maelewano mazuri kati ya Pique na Mina. Ni mara yao ya kwanza kujikuta kwenye hali ngumu kama ile. 

Mina anaweza kubeba lawama za mabao yote ya Levante. Bao la kwanza ni uzembe wa kushindwa kumkaba Jose Luis Morales aliyekuwa huru na kutengeneza nafasi kwa mfungaji. 

Bao la pili ni uzembe ule ule wa kushindwa kumkaba Emmanuel Boateng, ambaye alikuwa huru kwenye boksi na kufunga bao rahisi. Ni mara chache sana kuona Barca wakiruhusu mabao ya aina ile. 

Kosa jingine la Mina ni bao la tano. Kitendo cha kuchelewa kumkaba Enis Bardhi kilitoa nafasi kwa nyota huyo kutengeneza nafasi nzuri kwa Roger Marti aliyefunga kama anamnywesha mtoto uji. 

03: Kufungwa mabao ya haraka 

Mabao waliyofungwa Barcelona hasa katika kipindi cha pili yamepatikana ndani ya dakika saba. Huu ni uzembe wa aina yake kwa timu iliyotoka kubeba ubingwa wa La Liga wiki chache zilizopita. 

Uzembe huu wa kuruhusu mabao ya haraka uliwafanya mastraika wa Barca kuwa katika wakati mgumu wa kusawazisha. Walijitahidi sana lakini mwisho wa siku waliishia kufunga mabao manne tu. 

Kuruhusu mabao matatu ndani ya dakika saba kuliwapa mlima mkubwa sana Barcelona wa kupanda na kusaka matokeo. Hili liliwaumiza sana. 

Ni mchezo mbaya katika mioyo ya mashabiki wa Barca lakini ni dakika 90 nzuri kwenye kichwa cha Ernesto Valverde. 

Kutoka pale atakuwa amejifunza nini cha kufanya msimu ujao. Ni eneo gani linahitaji maboresho ya haraka na kubwa zaidi ni jinsi ya kuifanya Barca icheze katika ubora wake bila staa wao, Lionel Messi.

No comments:

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
Powered by Blogger.