Header Ads

MAPYA NDANI YA JANGWANI>>LWANDAMINA NDIE CHANZO CHA YANGA KUFANYA VIBAYA MECHI ZAKE ZOTE,




Wakati Yanga ikishindwa kutamba katika uwanja wake wa nyumbani baada ya kulazimishwa sare na Rayon Sports ya Rwanda kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya 
makundi, kocha mkuu wa zamani wa kikosi hicho, George Lwandamina, ametajwa kama ndiye chanzo cha kikosi hicho kufanya vibaya katika michezo yao ya hivi karibuni. 

Lwandamina, ambaye alikuwa akisaidiana na Shadrack Nsajigwa, aliamua kutimka zake na kujiunga na timu yake ya zamani ya Zesco United ya nchini kwao Zambia. 

Licha ya kwamba hata kabla ya kuondoka, kikosi hicho kilikuwa kikikabiliwa na matatizo mengi, likiwamo la ukata, lakini walikuwa wakijikongoja na kupata matokeo mazuri, tofauti na sasa. 

Tangu kuondoka kwa Mzambia huyo, kikosi hicho kimecheza michezo nane bila kupata ushindi wowote, hiyo ikiashiria kuwa, kuna namna kocha huyo alikuwa akiishi na wachezaji wake kiasi kwamba walikuwa wakicheza kwa moyo. 

Baadhi ya wachezaji wa Yanga Kwa njia ya simu wameiambia BongoFC kuwa, Lwandamina alikuwa akiishi nao kama mzazi, huku akiwapa maneno ya faraja ambayo yaliwafanya kupambana ndani ya uwanja, tofauti na sasa. 



“Hata wakati Kocha Lwandamina yupo tulikuwa na matatizo ya kutokulipwa mishahara, lakini alikuwa akitukalisha chini na kutuambia tupambane, kwani tunaweza tukaonekana timu nyingine ndani na nje ya nchi tukasajiliwa. 

“Yaani tulimchukulia kama mzazi, tofauti na sasa, kwani hakuna aliyeweza kuvaa vizuri viatu vyake, ndiyo maana unakuta hata baadhi wanafika hatua ya kugoma,” alisema mmoja wa wachezaji waandamizi wa kikosi hicho. 

Mchezo wa mwisho kwa Lwandamina kuiongoza Yanga ilikuwa ni dhidi ya Welayta Dicha ya Ethiopia, mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na Wanajangwani hao kushinda mabao 2-0. 

Katika michezo hiyo sita waliyocheza bila Lwandamina, wamejikuta wakifungwa michezo minne na kutoka sare miwili. 

Michezo hiyo waliyotoka sare ni dhidi ya Singida United pamoja na Mbeya City, ambazo zote zilikuwa sare ya kufungana bao 1-1, na michezo waliyofungwa ni dhidi ya Welayta Dicha ya Ethiopia mchezo wa Kombe la Shirikisho, wakilala bao 1-0. 

Michezo mingine ni dhidi ya Simba, wakifungwa bao 1-0, wakafungwa tena mabao 4-0 dhidi ya USM Alger ya nchini Algeria, mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi na pia kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Prisons na suluhu ya 0-0 kwenye mchezo wa jana dhidi ya Rayon Sports katika Kundi B la michuano ya kombe la shirikisho Afrika. 

Hata hivyo kwa sasa Yanga, imeendelea kushika mkia kwenye kundi lao wakiwa na pointi moja tu kutokana na kushindwa kutamba katika mechi zao zote mbili walizocheza. 

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya mashabiki wa Yanga wamefikia hatua ya kusema kama Lwandamina angekuwapo wasingeendelea kupata aibu hii wanayoipata kwa sasa.

No comments:

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
Powered by Blogger.